UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
INSTITUTE OF KISWAHILI STUDIES (IKS)

BARUA ZA SHAABAN ROBERT 1931-1958

Barua za Shaaban Robert ni mkusanyiko wa barua na nyaraka nyingine kama 100 za Shaaban Robert, au zinazomhusu Shaaban Robert  (1909-1962). Zaidi ya nusu ya nyaraka hizo ni barua ambazo mwandishi  na mshairi huyo mashuhuri wa Afrika Mashariki wa kipindi cha ukoloni, alimwandikia mdogo wake, Bwana Yusuf Mwinyiulenge (Ulenge), kati ya mwaka 1931 na 1958. Barua hizi zilihifadhiwa na Bwana Yusuf Ulenge kwa Zaidi ya miaka 50 hadi alipozikabidhi kwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili mwaka 1993. Baadhi ya nyaraka hizi zilipata kuchapishwa zamani katika Mambo Leo na magazeti mengine ya kipindi hicho cha ukoloni, lakini zilizonyingi hazijapata kuchapishwa.

 

Kitabu hiki kina umhimu wa pekee katika taaluma na historia ya fasihi ya Kiswahili. Mbali na kutupatia taarifa kuhusu ukoo wa Shabaan Robert na Yusuf Ulenge, na kuhusu uhusiano wao wa kipekee, kitabu hiki kinatupa taarifa za Zaidi kuhusu haiba ya Shaaban Robert, mawazo yake na namna yalivyojengeka katika ujana wake. Hapana shaka kuwa barua hizi zitakusaidia kuzielewa vizuri Zaidi katika kazi maridhawa za Shabaan Robert, kwani zinatoa taswira nyingine isiyofahamika ya shaha huyo wa malenga wa lugha wa Kiswahili.  Aidha zitatupa picha Fulani ya hali ya maisha na matatizo ya kiuchumi na kijamii ya kipindi cha ukoloni, hasa miaka ya 1930-1950, nchini Tanganyika na Afrika Mashariki kwa ujumla.

 

Kitabu hiki kitawafaa watafiti wa lugha na fasihi ya Kiswahili, wanafunzi na walimu wa vyuo vikuu na vyuo vya walimu, walimu na wanafunzi wa sekondari, watunzi wa hadithi na mashairi, na wananchi wote kwa ujumla wapendao kujielimisha kuhusu mwandishi huyu muhimu.