FURSA ZA UWEKEZAJI NA UTOAJI WA HUDUMA KATIKA KAMPASI MPYA YA UDSM KAGERA
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinapenda kuufahamisha umma, taasisi za umma na binafsi, makampuni, wafanyabiashara na watoa huduma kuhusu fursa za uwekezaji na uendeshaji wa biashara zinazopatikana katika Kampasi mpya ya UDSM Kagera, eneo la Kwauso katika vijiji vya Itahwa/Kangabusharo, Wilaya ya Bukoba, Mkoa wa Kagera.
Kampasi inatarajiwa kuanza shughuli za kitaaluma katika mwaka wa masomo 2026/2027 ikiwa na takribani wanafunzi 200 katika hatua ya awali, pamoja na watumishi, wageni na watumiaji wengine wa Kampasi. Kadiri shughuli za Kampasi zitakavyopanuka, idadi ya watumiaji na mahitaji ya huduma mbalimbali yanatarajiwa kuongezeka.
Katika maandalizi ya kuanza kwa shughuli za Kampasi na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa jamii ya Chuo, UDSM inawaalika watu binafsi, makampuni na wafanyabiashara wenye sifa, uwezo na nia ya kuendesha biashara katika Kampasi kuwasilisha maombi yao. Kuna makundi mawili ya uwekezaji: kundi la kwanza ni fursa ambazo zinaombwa kwa kujaza fomu maalum na kundi la pili ni fursa zinazoombwa kupitia Mfumo wa Taifa wa Ununuzi kwa Njia ya Kielektroniki (NeST)
Makundi maalum (vijana, wanawake na wenye ulemavu) wanahamasishwa kushiriki katika fursa hizi.