UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
RESEARCH AND EDUCATION FOR DEMOCRACY IN TANZANIA (REDET)

Announcements

Hii ni taarifa ya awali iliyoandaliwa na Tanzania Election Monitoring Committee (TEMCO) kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura (PNVR) uliofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipa Tume jukumu la kusimamia na kuratibu uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani katika Jamhuri ya Muungano. Zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ni sehemu muhimu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 2020. Uboreshaji wa daftari hilo ulihusisha shughuli kuu nne, uandikishaji wapiga kura wapya ambao wametimiza umri wa miaka 18 na wengine ambao watafikisha umri huo mwezi Oktoba. Ulihusisha pia watu ambao wamehamia maeneo mengine ya makazi na walipenda kuamishia taarifa zao huko. Zoezi hili lilitoa fursa kwa wapiga kura ambao vitambulisho vyao vimeharibika au kupotea kupata vitambulisho vipya. Mwisho, zoezi la kuandikisha wapiga kura lilihusisha kuwaondoa kutoka kwenye daftari la kudumu la wapiga kura watu waliopoteza sifa za kuwa wapiga kura, kama watu waliofariki.

 

Tangu zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura lianze tarehe 18 Julai 2019 mikoa 26 ya Tanzania Bara na mikoa 5 ya Zanzibar tangu zoezi lilipozinduliwa rasmi tarehe 18 Julai, 2019 mkoani Kilimanjaro. Kwa mujibu wa kifungu cha 40(1) cha Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (zilizochapishwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 792 na 793 tarehe 28 Desemba 2018) na kifungu cha 42(1) cha Kanuni za Serikali za Mitaa za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura za mwaka 2018, Tume iliialika TEMCO kuangalia zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura. TEMCO ilianza kuangalia uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura tarehe 1 Desemba 2019 na ilifanya kazi hiyo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa 89 katika mikoa 16 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Kwa mantiki hiyo, taarifa hii inajumuisha mikoa 16 ya Tanzania, pamoja na mikoa mitano ya Zanzibar, Mamlaka 89 za Serikali za Mitaa na vituo 614 vya kuandikisha wapiga kura. Taarifa hii imegawanyika katika sehemu sita, pamoja na utangulizi. Sehemu ya pili inajikita kwenye methodolojia. Sehemu ya tatu inahusu utoaji wa elimu ya mpiga kura. Sehemu ya nne inaangalia upatikanaji na utoaji mafunzo kwa maafisa walioandikisha wapiga kura. Mchakato wa kuandikisha wapiga kura unatazamwa katika sehemu ya tano ya taarifa hii. Sehemu ya sita inatoa hitimisho na mapendekezo.

Attachment: Download