UDSM Yaendelea Kukuza Fasihi ya Kiswahili, Tuzo za SAFAL Zikiadhimisha Miaka 10
Na Selemani Nambimbi, CMU
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeendelea kuonesha dhamira yake ya kukuza lugha na fasihi ya Kiswahili kwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya miaka 10 ya Tuzo za SAFAL Kiswahili Prize for African Literature, ambazo zimekuwa zikihamasisha waandishi barani Afrika kuandika kwa Kiswahili.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika Julai 24, 2026 katika Ukumbi wa Maktaba Mpya wa UDSM na kuhudhuriwa na wanataaluma, waandishi, wachapishaji, watunga sera na wadau wa fasihi kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Tuzo za SAFAL Kiswahili zilianzishwa mwaka 2014 na Dkt. Lizzy Attree pamoja na Prof. Mukoma wa Ngũgĩ baada ya kubaini kuwa hakukuwa na tuzo kubwa ya kimataifa iliyokuwa ikitambua kazi za fasihi zilizoandikwa kwa Kiswahili. Tangu kuanza kutolewa mwaka 2015, tuzo hizo zimepokea zaidi ya miswada 1,600, zimetambua washindi 40 na kusaidia kuchapishwa kwa vitabu zaidi ya 20.
Mwaka huu, zaidi ya miswada 200 iliwasilishwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika katika makundi ya riwaya, ushairi na hadithi fupi, jambo linaloonesha kuwa waandishi wengi zaidi wanaendelea kutumia Kiswahili katika kazi zao za ubunifu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi ambaye ni Waziri wa Habari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma, aliwataka serikali, sekta binafsi na wadau wengine kuendelea kuwekeza katika kukuza fasihi ya Kiswahili.
“Nawahimiza waandishi wote, hata wale ambao bado hawajawa maarufu, kushiriki katika tuzo hizi. Fasihi ni hazina ya mawazo ya jamii na waandishi ndiyo wanaohifadhi historia na utamaduni wetu. Kushiriki tu ni hatua muhimu”, alisema.
Kuhamasisha matumizi ya lugha za Kiafrika
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Tuzo za SAFAL Kiswahili, Prof. Abdilatif Abdalla, alisema lengo la tuzo hizo si kutambua waandishi bora pekee, bali pia kuhamasisha matumizi ya lugha za Kiafrika, hasa Kiswahili, pamoja na kukuza tafsiri za kazi za fasihi katika lugha mbalimbali.
Alisema fasihi ya Kiswahili ina nafasi muhimu katika kuhifadhi historia, maadili na utamaduni wa Waafrika, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuwaunga mkono waandishi na watafsiri.
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Biashara wa SAFAL Group, Anthony Ng’ang’a, alisema kampuni hiyo itaendelea kuunga mkono maendeleo ya fasihi ya Afrika. Alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, SAFAL Group imewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni moja katika uendeshaji na maendeleo ya tuzo hizo.
“Kwa miaka kumi iliyopita, tuzo hizi zimekuwa zikitambua waandishi wapya, kusaidia uchapishaji wa kazi zao na kufanya fasihi ya Kiswahili iwafikie wasomaji wengi zaidi barani Afrika na duniani,” alisema.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), kinaendelea kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza katika kufundisha na kufanya tafiti za Kiswahili barani Afrika. Kupitia ushirikiano wake na SAFAL Group pamoja na wadau wengine, chuo kinaendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza Kiswahili, kuendeleza tafiti za fasihi na kuwajengea uwezo waandishi na watafiti.
Ushirikiano huo unaendelea kuimarisha nafasi ya Kiswahili kama lugha ya elimu, ubunifu na maendeleo, huku ukiwalea waandishi na wasomi wa kizazi kipya barani Afrika.