Mlimani Media Yang’ara Kimataifa, Yatwaa Tuzo Maalum ya Kuendeleza Kiswahili
Na Mwandishi Maalum, SJMC
Chombo cha Habari cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mlimani Media, kimeendelea kuweka alama ya mafanikio katika tasnia ya habari baada ya kutunukiwa tuzo maalum kwa mchango wake mkubwa katika kukuza, kueneza na kuenzi lugha ya Kiswahili.
Tuzo hiyo ilitolewa katika Kongamano la 5 la Idhaa za Kiswahili Duniani, lililofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 24 hadi 27 Machi 2026 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), jijini Arusha.
Kongamano hilo limewakutanisha wadau wa lugha ya Kiswahili kutoka mataifa mbalimbali, likiwa na lengo la kujadili nafasi na mchango wa Kiswahili katika maendeleo ya kimataifa, hususan katika enzi ya utandawazi na mapinduzi ya kidijitali.
Hafla ya ufunguzi ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa serikali, ikiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, akishirikiana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, pamoja na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Riziki Pembe.
Tuzo hiyo inatambua mchango mahsusi wa Mlimani Media – ambayo inahusisha Mlimani TV, Mlimani Redio na Gazeti la The Hill Observer, yote yakiwa chini ya UDSM – katika kutumia majukwaa ya habari kama nyenzo ya kukifikisha Kiswahili kwa hadhira pana zaidi.
Kupitia vipindi vyake vya redio kama Amka na Mlimani, Pamoja na Kiswahili, pamoja na vipindi vya ushairi, na uwepo wake imara katika majukwaa ya kidijitali, Mlimani Media imekuwa kinara katika kuhamasisha matumizi fasaha ya Kiswahili, kukuza vipaji na kuibua maudhui bunifu yanayochochea ukuaji wa lugha hiyo.
Akizungumza wakati wa utoaji wa tuzo, Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Prof. Martin Mhando, alisisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi ya kimkakati katika kukuza na kulinda lugha ya Kiswahili.
Alieleza kuwa taasisi kama Mlimani Media zimekuwa mfano bora wa namna sekta ya habari inavyoweza kuchochea maendeleo ya lugha na utamaduni wa Kiafrika katika ngazi ya kimataifa.
Kielelezo cha ubora wa kazi inayofanywa na Mlimani Media
Kwa upande wake, Amidi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), Dkt. Mona Mwakalinga, ameeleza kufurahishwa kwake na mafanikio hayo, akibainisha kuwa tuzo hiyo ni kielelezo cha ubora wa kazi inayofanywa na Mlimani Media chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Tunajivunia mafanikio haya makubwa ambayo yanaakisi juhudi za kitaaluma na ubunifu wa wanafunzi na watumishi wetu. Hii ni ishara kuwa uwekezaji katika taaluma ya mawasiliano na matumizi sahihi ya Kiswahili unazaa matunda chanya,” alisema Dkt. Mwakalinga.
Aliongeza kuwa SJMC itaendelea kuimarisha ubunifu na tafiti zinazochangia maendeleo ya lugha ya Kiswahili na sekta ya habari kwa ujumla.
Naye Meneja wa Mlimani Media, ambaye pia ni Mhadhiri Msaidizi SJMC, Bw. Malika Nginila amesema kuwa tuzo hiyo ni chachu ya kuongeza juhudi katika kubuni na kusambaza maudhui yenye ubora wa juu wa lugha na maadili ya taaluma ya habari.
“Tunaahidi kuendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha Kiswahili kinapata nafasi stahiki katika vyombo vya habari vya kisasa na majukwaa ya kidijitali duniani”, alisema.
Kongamano hilo limeweka mkazo umuhimu wa mshikamano wa wadau katika kukuza na kulinda lugha ya Kiswahili ili iendelee kuwa chombo muhimu cha mawasiliano na utambulisho wa Afrika.
Kwa ujumla, tuzo hii ni heshima kubwa kwa Mlimani Media na inadhihirisha mafanikio ya juhudi za kitaifa na kimataifa za kukuza Kiswahili, ikiwa ni hatua muhimu katika safari ya kuhakikisha lugha hii adhimu inaendelea kustawi na kusambaa duniani kote.