Prof. Aldin Mutembei Ateuliwa Kuongoza Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika
Na Selemani Nambimbi, CMU
Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Aldin Mutembei, ameteuliwa kuongoza Makamishina tisa wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika chini ya Taasisi ya Kiafrika ya Lugha (African Academy of Languages - ACALAN), chini ya Umoja wa Afrika (AU), kwa kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2026 hadi 2030.
Kwa mujibu wa barua ya uteuzi huo kutoka ACALAN - taasisi inayosimamia maendeleo na uendelezaji wa lugha za Kiafrika, Prof. Mutembei atafanya kazi kwa kushirikiana na Makamishina wengine wa Kamisheni hiyo ya Kiswahili kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Makamishina hao ni Prof. Fikeni Senkoro (Tanzania), Prof. Kimani Njogu (Kenya), Prof. Inyani Simala (Kenya), Dkt. Kisembo Ronex Tendo (Uganda), Dkt. Aida Mutenyo (Uganda), Prof. Pacifique Malonga (Rwanda), Bw. Kitoko Moussa (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) na Prof. Denis Bukuru (Burundi).
Uteuzi wa Prof. Mutembei, ambaye ni Profesa wa Kiswahili na Fasihi, unakipa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nafasi muhimu katika juhudi za kimataifa za kuendeleza lugha ya Kiswahili na kuimarisha mchango wa Tanzania katika utekelezaji wa ajenda ya Umoja wa Afrika ya kukuza lugha za Kiafrika kama nyenzo za maendeleo, mshikamano na uhifadhi wa urithi wa kitamaduni wa bara.
Mkakati wa kukuza, na kulinda lugha za Kiafrika
ACALAN, ambayo ni taasisi muhimu na maalum ya Umoja wa Afrika, ilianzishwa mwaka 2001 kwa lengo la kukuza, kuendeleza na kulinda lugha za Kiafrika. Kupitia majukumu yake, taasisi hiyo hushirikiana na serikali, vyuo vikuu, taasisi za utafiti na wadau mbalimbali katika kuimarisha matumizi ya lugha za Kiafrika, ikiwemo Kiswahili, ambacho ni mojawapo ya lugha rasmi za kazi za Umoja wa Afrika.
Katika nafasi yake mpya, Prof. Mutembei ataratibu shughuli za Kamisheni ya Kiswahili kwa kusimamia utekelezaji wa programu na mikakati ya kuendeleza Kiswahili, kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama, kushiriki mikutano ya kimataifa na kuratibu juhudi zinazolenga kukuza Kiswahili kama lugha ya mawasiliano, elimu, utafiti, diplomasia na maendeleo barani Afrika.
Uteuzi huo unakuja wakati ambapo Kiswahili kinaendelea kupata hadhi kubwa katika majukwaa ya kikanda na kimataifa, hususan baada ya Umoja wa Afrika kukitambua kuwa mojawapo ya lugha zake rasmi za kazi. Hatua hiyo imeongeza fursa za matumizi ya Kiswahili katika diplomasia, elimu, biashara na ushirikiano wa kimataifa.
Kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uteuzi wa Prof. Mutembei ni uthibitisho wa mchango unaoendelea kutolewa na Chuo katika kufundisha, kufanya tafiti na kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania. Aidha, unaimarisha nafasi ya UDSM kama kitovu cha ubora katika taaluma, tafiti na maendeleo ya Kiswahili barani Afrika.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ushiriki wa Chuo katika programu na miradi ya kimataifa inayolenga kuimarisha matumizi ya Kiswahili, kukuza ushirikiano wa kitaaluma na kuendeleza diplomasia ya lugha kupitia mtandao wa ACALAN na Umoja wa Afrika.