UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
INSTITUTE OF KISWAHILI STUDIES (IKS)

MISINGI YA ISIMUJAMII

Mwandishi, Prof. Geoffrey Kitula King’ei ni Mhidhiri katika taaluma za Kiswahili zikiwemo: mbinu za matumizi ya lugha, uandishi wa kubuni, uchambuzi wa fasihi, ushairi na isimujamii. Tajiriba yake ndefu katika ufundishaji, uandishi na utafiti katika taaluma hizi imetamba takribani miaka thelathini sasa. Amewahi kuchapisha vitabu na Makala mbalimbali katika vipengele tofauti vya lugha na fasihi.

Katika misingi ya Isimujamii, matunzi amejitahidi kufafanua kwa mifano maridhawa baadhi ya dhana, istilahi na vipengee vya kimsingi katika somo la isimujamii. Katika miaka ya hivi karibuni, somo la isimujamii limepata umarufu mkubwa na limeanza kufundishwa kuanzia shule za sekondari, vyuo anuwai vinavyofundisha lugha na isimu na hasa katika vyuo vikuu. Mbali na Tanzania ambako taaluma ya isimu ya Kiswahili imekuwa ikifundishwa katika viwango tofauti kwa kutumia Kiswahili, katika mataifa mengine kama Kenya na Uganda, idadi kubwa ya vyuo vikuu vimekuwa vikifundisha taaluma hii kwa kutumia Kiingereza. Bila shaka, mpaka sasa, marejeleo mengi sana yanatumika kufunfishia isimujamii yameandikwa kwa Kiingereza. Hali hii hufanya ufundishaji kuwa  na ugumu maradufu: kusoma na kutafsiri pamoja na kufasiri maelezo yote kutoka Kiingereza hadi Kiswahili. Pili, kujaribu kulihusisha somo lenyewe na ufundishaji wake kwa kutafuta mifano mwafaka inayoakisi lugha na utamaduni wa Kiswahili na Kiafrika kwa ujumla. Kitabu hiki kimetilia maanani haja ya kurahisisha na kuboresha ufundishaji wa isimujamii kwa kutumia Kiswahili.

Baadhi ya maada muhimu zilizofafanuliwa katika kitabu hiki ni pamoja na: maana na mahusiko ya isimujamii; uanishaji wa lugha; usanifishaji na upangaji lugha; ukuzaji wa istilahi na hali ya lugha katika eneo la Afrika Mashariki. Tunatarajia kitabu hiki kitawapa msingi bora wanafunzi wa Kiswahili katika shule za sekondari, vyuo na vyuo vikuu vya Afrika Mashariki na kwingineko kinapofundiswa Kiswahili.

Kwa sasa, Prof. King’ei ni Profesa wa taaluma ya Kiswahili katika Idara ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika, Chuo Kikuu cha Kenyatta, Nairibi, Kenya.